Mwenyekiti wa Taasisi ya rais mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin William Mkapa HIV/AIDS Foundaation Meja jenerali mstaafu Herman Lupogo akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi pikipiki za kubebea wagonjwa na jengo la wazazi kijijini Ikungi.
Kikundi cha uhamasishaji cha kijiji cha Ikungi kikitoa burudani wakati wa hafla ya kukabidhi msaada wa pikipiki na jengo la wazazi Ikungi.
Mwenyekiti Lupogo (kushoto) akimkabidhi mkuu wa wilaya ya Singida,Pascal Mabiti funguo za pikipiki ya kubebea wagonjwa.
Taasisi ya rais mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin William Mkapa HIV/AIDS Foundation imetoa msaada wa zaidi ya shilingi milioni 219.3 kwa ajili ya kugharamia uboreshaji wa huduma ya afya katika wilaya ya Singida na Iramba.
Hayo yamesemwa na mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa taasisi hiyo Major generali mstaafu Herman Lupogo,wakati akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi pikipiki tatu za kubebea wagonjwa na jengo la wazazi lililopo kwenye kituo cha afya cha Ikungi wilayani Singida.
Alisema kati ya fedha hizo shilingi milioni 105,722,710/= zimetumika kukarabati jengo la wazazi (maternity) lililopo kwenye kituo cha afya cha Ikungi wakati shilingi milioni 21 zimetumika kununulia pikipiki tatu za kubebea wagonjwa.
Aidha mwenyekiti Lupogo alisema taasisi hiyo chini ya mradi wake wa kuokoa maisha ya mama wajawazito imetumia shilingi milioni 92,640,131/= kugharamia mafunzo na ununuzi wa vifaa mbalimbali.
“Taasisi yetu ikishirikiana na Ifakara health Institute chini ya ufadhili wa World Lung Foundation la nchini Marekani ilianza kwa kutoa mafunzo ya afya kwa watumishi 16 kutoka vituo vya afya vya Ikungi na kile cha Ndago wilayani Irmaba.Mafunzo hayo yalilenga katika kuwawezesha watumishi hao kutoa huduma bora za dharura ili kuokoa maisha kwa wajawazito na watoto wachanga”alifafanua mwenyekiti Lupogo.
Kwa upande wake mgeni rasmi mkuu wa wilaya ya Singida Pascal Mabiti, amewahimiza wanaume kujenga tabia ya kuwapeleka wake zao kliniki wakati wa kujifungua unapofika.
“Akina mama hao wapelekwe mapema kujifungua kwenye zahanati vituo vya afya na katika hospitali ili kama yapo matatizo,yaweze kushughulikiwa haraka kabla hayajasababisha madhara makubwa”alisema DC huyo.
Wakati huo huo, Mabiti aliwaagiza waganga na wauguzi mkoani Singida wakati wote wazingatie viapo vyao vya kazi ili kupunguza malalamiko yanayotolewa na wananchi mara kwa mara yakiwemo ya lugha chafu na kutokuwajali wagonjwa.
Kwa mujibu wa DC Mabiti, mwaka 2010 mkoa wa Singida ulikuwa na vifo vya watoto 454 sawa na uwiano wa watoto 11/1,000 ya uzazi hai.Manispaa ya Singida iliongoza kwa vifo 200 ikifuatiwa na halmashauri ya wilaya ya Singida,95,Iramba 90 na Manyoni 69.
0 comments:
Post a Comment