Friday, June 1, 2012

....LULU BADO NI NGOMA ZITO....


UPANDE wa Mashitaka katika kesi ya mauaji ya Steven Kanumba inayomkabili msanii wa filamu nchini, Elizabeth Michael Lulu, umepinga maombi yaliyowasilishwa Mahakama Kuu kuhusu umri wa mshtakiwa huyo na kuomba maombi hayo yatupiliwe mbali.

Pingamizi hilo la awali liliwasilishwa mahakamani hapo jana Jumatatu na mawakili wa upande wa mashitaka, Elizabeth Kaganda na Shadrack Kimaro mbele ya Jaji Dk. Fauz Twaib.

Akiwasilisha pingamizi hilo, Kimaro alidai kuwa maombi hayo yamewasilishwa mahakamani hapo kinyume cha sheria.

Alidai kuwa hata vifungu vya sheria namba 120 (ii) na 113 (i) na (ii) vya Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 ambavyo upande wa utetezi umevitumia kuwasilisha maombi hayo, haviipi mamlaka mahakama hiyo kuweza kusikiliza maombi hayo.

Ni kweli kwamba mahakama hii ina uwezo wa kusikiliza suala la umri, lakini namna upande wa utetezi walivyowasilisha maombi yao haiwezeshi mahakama hii kuweza kuyasikiliza,alidai Kimaro.

Kimaro alidai kuwa mojawapo ya kielelezo kilichowasilishwa na upande wa utetezi wakidai ni uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu si uamuzi bali ni amri ya mahakama.

Akijibu hoja hizo, Wakili wa utetezi, Kennedy Fungamtama, ambaye alikuwa akisaidiana na Fulgence Massawe na Peter Kibatala, alidai kuwa maombi yao ni ya msingi kwani wamefuata taratibu zote za kisheria na kuomba mahakama iyasikilize.

Tulichofanya tumefuata amri iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kilichoko hapa ni ubishi kuhusiana na umri wa mshtakiwa," alisema.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haikutoa uamuzi, bali ilitoa amri kwa mawakili wa mshtakiwa kama wana maombi yoyote wafanye hivyo kupitia Mahakama Kuu na ndivyo tulivyofanya.

Wakili huyo wa utetezi aliendelea kudai kuwa, hata katika Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 imetafsiri neno mahakama ikimaanisha kuwa ni ile ya Mwanzo, Wilaya, Mkoa ama Mahakama Kuu hivyo ni sahihi maombi yao kuwepo mahakamani hapo.

Upande wa mashitaka wameshindwa kuisaidia mahakama hii ni taratibu zipi ambazo hatukuzifuata katika kuwasilisha maombi haya, hivyo pingamizi lao litupiliwe mbali, alidai Fungamtama.

Baada ya kusikiliza hoja zote Jaji Twaib aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 11 mwaka huu atakapotoa uamuzi kuhusiana na maombi hayo.

Upande wa utetezi umewasilisha maombi hayo ukiiomba Mahakama Kuu iangalie na kuona kama Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ina uwezo wa kuamua suala hilo.

Hatua ya upande wa utetezi kwenda Mahakama Kuu ilikuja baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutupilia mbali maombi hayo.

Wakati wakiwasilisha maombi hayo Kisutu, Fungamtama alidai kuwa mteja wao ana umri wa miaka 17 na si 18 kama inavyotamkwa mahakamani.

Alidai kuwa hata cheti cha kuzaliwa walichokiwasilisha mahakamani kinaonyesha mahali na tarehe aliyozaliwa mshtakiwa hivyo kuwa na umri wa miaka 17.

Fungamtama alidai kuwa kulingana na Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 inatafsiri kuwa mtoto ni yule aliyekuwa na umri chini ya miaka 18 hivyo mteja wao alipaswa kushtakiwa katika Mahakama ya Watoto.

Lulu anayedaiwa kuhusika na mauaji ya Kanumba yaliyotokea Aprili 7 mwaka huu, bado anaendelea kusota rumande kutokana na kesi inayomkabili kutokuwa na dhamana.

0 comments:

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More

 
Design by Free WordPress Themes | Bloggerized by Lasantha - Premium Blogger Themes | Grants For Single Moms