Friday, April 6, 2012

.......VIJEMBE VYATAWALA KATI YA RASHID NA MANENO........


BONDIA mkongwe nchini, Rashid Snake Boy  Matumla ametamba kumburuza mpinzani wake, Maneno Mtambo wa Gongo Oswald katika pambano la raundi nane la uzani wa middle litakalofanyika keshokutwa kwenye Ukumbi wa Dar Live.

Matumla alikaririwa na televisheni ya Taifa, TBC juzi akisema: "Oswald ni bondia goigoi ambaye ameshindwa kutamba katika mapambano mengi dhidi yangu na kwa sasa nitamgeuza kama buldoza ili kumfanya asifikirie kupigana na mimi tena."

Alisema kuwa anajua kuwa anapigana na bondia ambaye hana kiwango cha mchezo huo na kushindwa kutamba kimataifa enzi za ujana wake na mpaka sasa amefikia umri wa kuitwa mzee.

Sidhani kama napigana na bondia mwenye kiwango siku hiyo, ila nawaomba mashabiki kufika kwa wingi ili kuona ninafanya nini kwake na ninaamini kamwe hatajaribu kuomba au kufikiria kuzichapa na mimi katika pambano la ubingwa au lisilokuwa la ubingwa, alisema Matumla.

Naye Oswald alisema kuwa Matumla anabebwa na majaji kila mara na kwa sasa atamchapa kwa knock out (KO) ili adhihirishe ubora wake.

Najua napigana na bondia ambaye hana uwezo zaidi ya kubebwa kila wakati na majaji, dawa yake nimeipata na nitamuonyesha kazi siku hiyo, alisema Oswald.

Mratibu wa mpambano huo, Juma Mbizo alisema mabondia hao watapanda kwenye jukwaa la ukumbi huo kufungua ukurasa mpya wa masumbwi kwenye ukumbi huo.

Alisema pia kutakuwa na mapambano ya utangulizi ambapo Furaha Mganda atazichapa na Jamhuri Said wakati Abass Ally wa Arusha atapanda ulingoni kuzichapa na Mchumia Tumbo.

Sambamba pambano hilo la masumbwi, pia kutakuwa na mpambano mkali kati ya Juma Nature na Jua Kali na burudani ya muziki wa taarabu kutoka kwa TOT, East Africa Melody, Mangweah na bendi ya FM Academia.

0 comments:

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More

 
Design by Free WordPress Themes | Bloggerized by Lasantha - Premium Blogger Themes | Grants For Single Moms