Yapata wiki tatu sasa tangu msanii
mwenzangu Steven Kanumba aage dunia, na kama ilivyo kwa kila kitu kinapotokea
huandamana na kila aina ya maneno na hisia mbali mbali kutokana na mitazamo ya
watu kupishana kuhusiana na jambo husika. Kulingana na muktadha huo, msiba wa
Steven Kanumba umekumbwa na maneno na hisia kama hizo, hususan mazingira ya
kifo chake; kinachosikitisha zaidi watu wengi (ambao wanajitambulisha kama
wapenzi wa Kanumba), na baadhi ya vyombo binafsi vya habari vimekuwa
vikinihusisha na kifo hicho, kwa kusema kwamba kwa njia moja au nyingine
ninahusika na mauaji ya Steven Kanumba. Kwa muda wote huo tangu msiba
ulipotokea mpaka leo hii nashika kalamu kujaribu kuyaweka sawa na kuondosha
hisia chafu katika fikra za watu, nimekuwa nikipitia katika wakati mgumu sana
kwa jinsi ambavyo nimekuwa nikinyooshewa vidole kila upande nikihusishwa na
kifo hicho, kiujumla nimezingatia maoni ya wapenzi ya mashabiki wangu
wakinitaka kuwa na subira, ila kuna ukweli usemao kwamba, uongo ukirudiwa
sana jamii huusadiki na kuuona ukweli, nimeona nisikae kimya ila niweke sawa
hili kwamba sihusiki na kifo cha Steven Kanumba.
Nasema wazi kwanza sihusiki kabisa
na kifo cha Kanumba kwanza kwa kuzingatia mazingira yenyewe ya kifo
kilivyotokea. Wakati kifo hicho kinatokea, nilikuwa sehemu nyingine kabisa na
mimi nilikuwa mtu wa tatu kutaarifiwa kwamba Kanumba amepatwa na mkasa ambao
baadae ulisababisha kifo chake. Na na hata nilipofika katika hospitali ya
Muhimbili (tofauti na watu wanavyodhani kuwa nilifika nyumbani kwake; ukweli
mimi nilimkuta tayari amepelekwa Muhimbili), nilikuta tayari alikuwa
ameshafariki ndio maana hata Polisi wanaohusika na usalama wa raia, si tu
kwamba hawakuniweka chini ya ulinzi, sikuitwa hata kuhojiwa kwa sababu hakuna
mazingira yoyote yanayonihusisha mimi na kifo hicho.
Pili, watu wanahusisha tofauti za
kibinadamu zilizokuwepo baina yetu na kifo hicho, nasema hii sio sahihi kwa
sababu kwanza ni kawaida kwa binadamu kutofautiana, isipokuwa kwetu sisi baadhi
ya vyombo vya habari vilikuwa vinakuza kwa sababu nisizozijua, hivyo jamii
ikachukulia kuwa tofauti zile ni uadui kitu ambacho sio sahihi, kwani sisi
hatukuwa watu pekee tunaotofautiana kwani huu ni mwenendo wa kawaida wa dunia;
hivi jana tumeshuhudia Waziri mmoja akieleza bayana katika mkutano na waandishi
wa habari kuwa na tofauti na naibu wake, lakini hatuajasikia ikiandikwa wana
‘bifu’ bali imetafutwa lugha nzuri ya kupamba tofauti hizo, kwa kuwa
waliohusika ni waheshimiwa, ila kwa wengine kutokana na sababu tusizozijua,
inaonekana kama ni haki yetu kuandikwa vibaya. Kinachosikitisha, kwa nini jambo
hili linachukuliwa kwa mkazo mkubwa sana, kwani hatujawahi kusikia watu wakiwa
wanatofautiana na ndugu jamaa hata na marafiki zao na inaonekana kawaida tu?
Kwani vyombo vya habari havikuwahi kuandika kuwa marehemu Steven Kanumba
alikuwa na tofauti na baba yake, na yeye mwenyewe alitamka hivyo katika vyombo
vya habari, mbona wameliongea bila kuongeza chumvi, na jamii inaona kuwa ni
jambo la kawaida la kibinadamu.
Pengine watu wanaojaribu kuongea
hayo, hawajui mimi na Steven Kanumba tumetoka wapi? Sisi si watu tuliokutana
barabarani, tuna historia katika kazi yetu ya sanaa na pia katika maisha maisha
yetu. Mwanzoni kabisa, mimi ndiye niliyempokea Kanumba pale Kaole na ndiye
niliyemfundisha sanaa pale (nadhani watu wanakumbuka tamthiliya za wakati huo
ITV) na baada ya hapo tulienda pamoja katika kampuni ya Game 1st
Quality pamoja na tukafanya filamu kama Johari, Sikitiko Langu, Dangerous
Disire na nyinginezo, na tuliendelea kuwa pamoja katika kampuni hiyo mpaka
tulipofanya filamu ya Oprah mwaka 2008 ambapo niliingia rasmi kufanya kazi za
kampuni yangu, lakini tuliendelea kuwa pamoja hata wakati nikiendelea na kazi
za kampuni yangu. Pia mimi nilikuwa wa kwanza kuanza kufanya kazi na Steps na
baadae Kanumba alipoanza kufanya kazi zake mwenyewe na kunikuta huko
tuliendelea kuwa pamoja kama siku zote. Kitu kikubwa kilichokuwa kinaendelea
baina yetu, ni kwamba tulijenga ushindani wa kuendeleza kazi mbele kwa kila
mmoja akitoa kazi, mwingine anamjibu, Isitoshe hata vitu vyetu binafsi
utaona kama kuna kufanana; kuna wakati Kanumba alinunua Toyota Ruv 4 nyeusi
mimi nikanunua ya kijani, aliponunua Harrier na mimi nikanunua pia, na hata
gari za hivi karibuni, ukitazama utaona kuwa zinafana kwa karibu; hii ilikuwa ni
kama maisha yetu, hatukuwa na uadui, ilikuwa tunapeana changamoto za maendeleo.
Watu wanaojaribu kuonesha
kuwa tofauti zetu ilikuwa ni uadui, huwa hawajui wapi tulikotoka ndio maana
wanasema wasemavyo na katika kuthibitisha kuwa tofauti hizo hazikufikia katika
uadui, kuna watu ambao wanafanya kazi nami katika kampuni yangu ya RJ ndio hao
hao Kanumba alikuwa anawatumia siku zote katika kazi zake, hata baada ya
tofauti hizo hakuna aliyekoma kufanya kazi na yeyote kati yetu. Hii
inathibitisha kuwa tofauti ilikuwa kati yetu kama binadamu, sio chuki za
kimafanikio, ingekuwa hivyo watu kama Junior Syaary ambaye mara nyingi hufanya
final editing katika RJ ndio huyo huyo alikuwa akifanya na Kanumba, Ally Yakuti
ambaye anaandika script za RJ, ndiye huyo huyo aliyekuwa anaandika kwa Kanumba,
Steven Shoo ambaye ni mtaalamu wangu wa light, ndiye huyo huyo anayetumiwa na
Kanumba na wengine wengi kama Juma Chikoka aliyecheza kikamilifu katika filamu
ya kijiji cha Tambua Haki, ambaye pia anashiriki filamu nyingi za RJ, na wote
hao, hawakuanzia kwa Kanumba, wote wameanza kwangu mimi ndio niliompatia na
hata baada ya hayo yanayosemwa kuwa kuwa ni uadui, sikuwahi kuwakataza kufanya
kazi na Kanumba.
Tatu kumtuhumu mtu kwa namna
yoyote ile bila ya uthibitisho wa tuhuma hizo, ni kosa kwa sheria za nchi na
pia kama ni mfuasi wa dini yoyote ni dhambi, kwani wakati ukisema hayo huku
hujui uhalisia bali unasukumwa na nguvu za hisia tu ni sawa na kumchafua mtu
huyo katika jamii bila ya kujua jamii inamchukuliaje. Napenda kusema wazi wazi
kuwa, kwa kila anayetekwa na wimbi hili, ajaribu kufikiria leo ipo kwangu mimi,
kesho inaweza kuhamia kwako, kwani mimi sio wa kwanza kufikwa na haya, inaweza
kukukuta hata wewe au ndugu yako, utajisikiaje. Na kama kweli mimi nimehusika
na kifo cha Kanumba kwa namna yoyote ile, basi Mungu atanihukumu na kila aliye
hai atashuhudia, ila kama sijahusika kwa lolote, Mungu hatonihukumu na badala
yake ataniinua, kwa kuwa ninapita katika kipindi kigumu mno sasa hivi kwa
madhila haya.
Mwisho kabisa napenda kumaliza kwa
msemo usemao, ajidhaniaye amesimama, aangalie asianguke, kwani kadri mambo haya
yanavyoendelea, usidhani yataishia kwangu, kwani mkono wa dhuluma haushii
karibu, ukisikia jirani anapiga kelele za mwizi, usilale kamsaidie, usiseme
kuwa hatuhusiki kwani hayupo kwetu, kesho utafikwa na wewe utakosa wa
kukusaidia. cha msingi kama tunampenda sana ndugu yetu ni kumuombea kwa Mungu,
kwani hatujui makao yake huko aliko, na sio kuunda vitu ambavyo kamwe hata yeye
angekuwa hai asingeviafiki.
MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU
STEVEN KANUMBA MAHALI PEMA PEPONI
MUNGU IBARIKI AFRIKA MUNGU IBARIKI
TANZANIA
Source: ray the greatest blog
0 comments:
Post a Comment