Tuesday, October 9, 2012

.....RICK ROSS AWAASA VIJANA......


DAKIKA 45 alizozitumia mwanamuziki kutoka nchini Marekani, William Leonard Roberts, Rick Ross akiwa jukwaani aliweza kuburudisha na kuelimisha maelfu ya vijana waliojitokeza katika Tamasha la Serengeti Fiesta lililofanyika usiku wa kuamkia jana katika Viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam.

Rapa huyo anayeshika nafasi za juu kati ya wanamuziki wa kimataifa hivi sasa, alisikika mara kwa mara akiwataka vijana kujituma katika kufanya kazi kwa bidii ili kuyafikia mafanikio kwa njia za halali.

"Unatakiwa kufanya kazi mwanamume, fanya kazi jitume na teseka katika kutafuta maisha, mimi ni boss, lakini nilikuwa boss kabla sijapata maisha, nilijituma katika kutafuta," ni maneno aliyoyarudia mara kwa mara Rick Ross kila alipomaliza kuimba nyimbo.

"Ninahisi upendo wa hali ya juu, hii ni mara yangu ya kwanza kufika katika nchi hii ya watu wakarimu, najua nchi itazidi kupata maendeleo na baadaye mtafikia malengo ikiwa vijana mtajituma," alisema mwanamuziki huyo mwenye miaka 36, ambaye aliimba vibao kama The Boss ft T.Pain, Hustlin, Aston Martin Music, I m ma Boss, Blow Money Fast (BMF) na nyinginezo nyingi.

Rick Ross ambaye alipanda jukwaani saa nane na dakika 20 usiku alifurahiwa zaidi na mashabiki ambao awali walimwona Rick Ross bandia (Mtanzania anayefanana na Rick Ross) aliyepanda saa saba kamili usiku huo.

Rick Ross aliimba vibao vyake vilivyopo kwenye chati pekee na kushuka jukwaani saa tisa na dakika tano usiku huku mashabiki wakiwa bado wana kiu ya kuendelea kusikiliza baadhi ya vibao vyake vilivyosalia.

Msanii Mwasiti Almasi alipata wakati mgumu baada ya kupokea kijiti kutoka kwa Rick Ross hali iliyomfanya aimbe kwa kutetemeka jukwaani huku baadhi ya mashabiki wakijikusanya na kutoka uwanjani.

Kupungua kwa mashabiki kulileta ahueni kwa baadhi ya mashabiki kwa sababu awali Leaders ilikuwa imejaa watu wengi, huku wasanii wengine waliokuwa wamesalia wakiendelea kutoa burudani.

Katika tamasha hilo usalama ulizingatiwa sana na kulikuwa na askari zaidi ya 250 ambao walikuwa wamezagaa hivyo kuhakikisha usalama wa kutosha kwa raia.

Mazingira ya uwanja yalikuwa salama ingawa kulikuwa na hatari kutokana na uwanja kujaa kupita kiasi na watu walikuwa wakisukumana ovyo mara baada ya Rick Ross kupanda jukwaani.

Burudani hiyo ilifunguliwa na Kundi la Makomandoo kabla ya kumpisha Rich Mavoko, Recho, Linah, TID, Nay Wa Mitego, Mwana FA, Stamina Wanaume Family, AT, Shilole, Nikki wa Pili na Joh Makini kabla ya kupanda jukwaa Rick Ross.

Baada ya mwanamuziki Rick Ross kuimba alimwachia kijiti Mwasiti, Dayna, Fid Q, Quick Rokar, Country Boy, Darasa, Sheta, Mabeste, Juma Nature, Nuru, Ommy Dimpoz, Diamond na wengineo.

0 comments:

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More

 
Design by Free WordPress Themes | Bloggerized by Lasantha - Premium Blogger Themes | Grants For Single Moms