Monday, July 2, 2012

......NIMEPATA KITU ORIJINO NA CHA UKWELI......

MSANII machachari wa Bongo Flava, Bob Junior a.k.a Rais wa Masharobaro, anaachana na kambi ya ukapera na kuanza maisha mapya atakapofunga ndoa kesho Jumapili.

Msanii huyo aliyetamba na nyimbo za 'Oyoyo', 'Andazi', 'Mapenzi ya Kweli' pamoja na 'Nichumu' zinazoendelea kusumbua katika vituo mbalimbali vya redio na runinga ndani na nje ya Tanzania, amesema ameamua kuvuta jiko kwani wakati wake umefika.

Akizungumza na Mwanaspoti, Bob alisema: "Huu ni muda wa kupata mwenzangu nitakayeshirikiana naye kwa kila jambo. Ninafanya hivi ili kujiepusha na anasa za dunia maana mambo ni mengi.

Anafafanua kuwa mwanamke anayetarajia kumwoa amekidhi vigezo ambavyo yeye binafsi anavihitaji kwa mke.

"Ndoa si kukurupuka. Nimekuwa makini mno kufikia uamuzi huu ili kuepusha migongano au migogoro ndani ya ndoa, nimechagua mwanamke ambaye naona kabisa amekidhi vigezo ninavyohitaji na mwenye tabia ambazo tunaendana, alisema.

Akivitaja vigezo hivyo anasema siku zote alihitaji kuwa na mke mwenye tabia njema, aliyelelewa katika maadili na misingi ya dini yake ya Kiislamu na mwenye kupenda kumcha Mungu.

Anasema ingawa katika hali ya kawaida ni ngumu kumpata mwanamke mwenye vigezo hivyo, lakini kwa upande wake amebahatika kumpata mwanamke huyo kutoka visiwani Zanzibar.

Nimelelewa katika misingi ya Kiislamu na ndiyo maana nahitaji mke ambaye pia atakuwa amejengwa vizuri katika misingi hiyo ili aweze kunisukuma niweze kumcha Mungu kama ilivyokuwa awali," alisema.

"Unajua kidogo siku hizi nimetawaliwa na mambo ya dunia sasa lazima kuwa na mtu atakayesaidia kuniweka sawa."

Anasema kutokana na hilo hapo kesho anatarajia kupanda boti mpaka visiwani Zanzibar ambapo ataenda kufunga ndoa na baadaye kumtambulisha rasmi mkewe kwa mashabiki wake kwenye shoo maalum itakayofanyika katika klabu ya Billicanas iliyopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

Nitapangilia kila kitu kwa muda wake kwani natakiwa nisiwanyime burudani mashabiki wangu na vilevile lazima niwajibike kwa mke wangu," aliongeza.

"Nina uhakika kwa kupanga ratiba vizuri, nitamudu bila wasiwasi wowote, naweza kusema ndoa itanipa changamoto ya kutafuta zaidi ili kuhakikisha familia ninayokwenda kuianzisha inapata mahitaji yote muhimu, mwanaume lazima uimudu familia.

Licha ya kuwa mwanamuziki, Bob Junior pia ni mtayarishaji wa muziki katika studio yake inayoitwa Sharobaro Records ambayo imefanikiwa kutengeneza nyimbo mbalimbali.

Miongoni mwa nyimbo zilizopita katika mikono yake ni pamoja na 'Lofa' ya Top C, 'Kamwambie' ya Diamond, 'Far Away' ya Big Jahman na nyinginezo kadhaa.

0 comments:

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More

 
Design by Free WordPress Themes | Bloggerized by Lasantha - Premium Blogger Themes | Grants For Single Moms