Friday, June 15, 2012

.....MAMBO YAIVA, WAREMBO MISS TANZANIA WAJINADI.....


WASHIRIKI wa Shindano la Redds Miss Tanzania wametamba kuiwakilisha vyema Tanzania katika shindano la dunia litakalofanyika Mongoria huko China Agosti 18.

Jumla ya warembo kumi waliingia kambini juzi kujiandaa na shindano la kutafuta mshindi atakayeiwakilisha Tanzania katika mashindano ya dunia.

Shindano la kumtafuta miss Tanzania litafanyika keshokutwa kwenye ukumbi wa 327 club.

Wakizungumza katika kambi yao iliyopo katika hoteli ya Girrafe washiriki hao walisema licha ya muda mchache wa maandalizi, lakini wana imani kubwa kuwa Tanzania itapata mwakilishi bora atakayeitangaza vema nchi katika mashindano ya dunia.

"Ni muda mchache wa maandalizi kama mlivyosikia mwaka huu mashindano ya dunia yamerudishwa nyuma badala ya mwezi wa kumi sasa ni mwezi wa nane hivyo tunahitaji kujianda kwa kipindi kifupi ingawa matumaini yetu ni makubwa kwani tunajiamini vya kutosha na lazima mwaka huu Tanzania ifike mbali,"alisema Lisa Jensen.

Naye Pendo Laiser ambaye ni Miss Tanzania namba mbili 2008 alisema wanajipanga kuhakikisha Tanzania inapeleka mwakilishi ambaye sio msindikizaji tu na badala yake itawakilishwa na mshiriki ambaye ana upeo mkubwa katika mambo ya urembo na kuiletea sifa nchi yake.

"Tumekuwa kila mwaka tukiwa wasindikizaji, lakini nataka kuwatoa hofu mashabiki wa fani hii ya urembo nchini kote kuona kuwa na sisi ni sehemu ya kuitangaza nchi na tunakwenda kwa nia moja ya kuwa katika nafasi nzuri katika mashindano hayo,"alisema Jenifer Kakolaki.

Warembo watakaochuana keshokutwa kwa ajili ya kumpata mshindi ni pamoja na Lisa Jensen, Pendo Laiser, Jenifar Kakolaki, Gloryblanca Mayowa, Hamisa Hassan, Queen Saleh, Christine Willium, Mwajabu Juma, Neema Saleh na Stella Mbuge.

Kuwahi kwa mashindano hayo ya dunia kumekuja baada ya kubadilika kwa kalenda ya mashindano ya dunia.

0 comments:

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More

 
Design by Free WordPress Themes | Bloggerized by Lasantha - Premium Blogger Themes | Grants For Single Moms