Saturday, May 5, 2012

.......NIMEJIAJIRI NA NIMEAJIRIWA......

MSANII anayeongoza nchini Tanzania kwa ubunifu wa kufanya shoo nzuri na zenye mvuto mkubwa kwa mashabiki wake amesema kuwa kwake muziki ni ajira na ni kazi kama ilivyo kwa mfanyakazi anayeingia ofisini.

Mshindi huyo wa tuzo tatu za Kilimanjaro kwa mwaka huu na mwaka 2010, alisema kuwa anafanya kazi hiyo kwa malengo zaidi na ndio maana anaweza kuwateka mashabiki wake na kuufanya muziki wa kizazi kipya uzidi kupendwa ndani na nje ya nchi.

"Nafanya muziki kama kazi, sifanyi muziki kujifurahisha mimi na kutafuta pesa pekee huku nikiwaacha mashabiki zangu hawajakata kiu ya burudani," alisema Diamond.

Alisema kikubwa hasa anachokifanya ni kushirikiana na watu na siku zote anaamini kuwa hawezi kufanya kazi peke yake pasipo kuwa na wacheza shoo wake kwani ndio wanaompa sapoti kubwa na kubadilishana mawazo ili kuleta vionjo vipya.

"Unajua mimi sina ubahili hasa ninapofanya kazi, na hili ndilo lililonifanya nizidi kusonga mbele katika kazi ya muziki ili upate ni lazima utoe, ili nifurahishe mashabiki ni lazima nizingatie kanuni kama hizi," alisema.

Diamond aliongeza kuwa maandalizi ni silaha nyingine ambayo inamfanya kila siku mashabiki wamwone mpya. "Siwezi kutokeza machoni mwa mashabiki nikiwa hivyo hivyo kila siku hata nikiwa na wimbo mpya sidhani kama watanifurahia kila siku staili hizo hizo, pia namtanguliza Mungu katika kila jambo," alisema.

Hata hivyo amewashukuru mashabiki na kuahidi kutowaangusha "nawashkuru sana na nawaahidi kuwa sitowaangusha na wategemee vitu vipya".

Wikiendi iliyopita msanii huyo alifanya shoo katika sehemu ya kiburudani ya Dar Live iliyopo jijini Dar es Salaam na kuvunja rekodi kwa kuingiza mashabiki wengi zaidi kuliko shoo zote zilizowahi kufanyika sehemu hiyo

Diamond ambaye alivaa mavazi ya kibaharia aliwasili eneo hilo kwa usafiri wa helikopta na hatimaye kuingia katika gari aina ya benzi ambalo lilimsogeza mpaka jukwaani.

Licha ya mvua kubwa iliyonyesha mashabiki walionekana kujifunika viti vyao kichwani ili waweze kuona utumbuizaji wa msanii huyo.

0 comments:

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More

 
Design by Free WordPress Themes | Bloggerized by Lasantha - Premium Blogger Themes | Grants For Single Moms