Friday, January 6, 2012

...MWANAMUZIKI ANAYEJALI ELIMU HUYU HAPA......

NI mwimbaji mwenye umaarufu mkubwa nchini na hata barani Afrika hasa baada ya kushinda tuzo ya MTV Africa (MAMAs).
Pia anaorodheshwa miongoni mwa wanamuziki tajiri nchini Kenya siyo kwa sababu ya mauzo ya muziki wake tu, bali pia malipo ya matangazo mbalimbali anayoshiriki.
Huyu ni msanii Wahu Kagwi ambaye licha ya kuwa na sifa kem kem, ni mwimbaji wa kufikiwa kwa urahisi akiwa hana majivuno.
Kwa Kenya Wahu hahitaji kutambulishwa. Kama hujuiona sura yake kwenye vyombo vya habari hasa televisheni akiimba au kuandaa kipindi cha Sakata (Citizen TV), basi utaiona katika mabango akitangaza bidhaa za kampuni mbalimbali.
Pia Wahu ni mfano bora. Anaiheshimu ndoa yake na msanii Nameless tofauti na wasanii wengine ambao baada ya kupata umaarufu ndoa zao huharibika.
Ni msomi mwenye Shahada ya Hesabu kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi na sasa anasomea Uzamili katika masuala ya uandishi wa habari katika chuo hicho.

Kimuziki licha ya mafanikio makubwa aliyopata, bado anasema yuko tayari kupokea ushauri wowote.
Amekuwa akitamba mno kwa vibao kama Sweet Love, Liar, Little Things You Do (wimbo aliomshirikisha Bobi Wine) na Still A Liar.
Wimbo wa Sweet Love uliibuka maarufu punde tu alipoutoa mwaka 2008 na anasema kwamba aliutunga miaka miwili nyuma alipokuwa mjamzito.
Kibao Still A Liar amekitoa hivi karibuni na anasema katika wimbo huo anawalenga wanaume ambao hata baada ya kuoa, bado hujihusisha na mapenzi nje ya ndoa zao.
Ni tatizo katika jamii, wanaume wa namna hii wanapaswa kuacha tabia hizo,anasema kuhusiana na wimbo huo uliorekodiwa katika studio ya RKay jijini Nairobi.

Anasema wimbo huo hauhusiani na ndoa yake. Mimi sijaathiriwa, lakini ninafahamu kwamba kuna ndoa kadhaa zilizo na matatizo ya namna hii. Mara nyingi tatizo huwa ni wanaume.
Licha ya kwamba umetolewa wiki mbili pekee zilizopita, tayari kibao hicho kimekuwa maarufu na kinachezwa kwenye vituo mbalimbali vya redio.
Ninayo imani wimbo huu utafanya vyema kama ilivyokuwa kwa zilizotangulia, anasema Wahu ambaye hakuwa ametoa kibao muda mrefu.
Kuhusiana na hilo, anasema ni kwasababu alikuwa bize na masomo.
Anasema kujikita kwake kwenye masomo hakumaanishi kuwa anataka kuachana na muziki.
Nasomea uandishi wa habari kwasababu nimewahi kufanya kazi hiyo katika kituo cha K24. Vyote viko ndani ya damu yangu,anasema.
Anaongeza kuwa kulingana na ulimwengu wa sasa wenye ushindani, ni vizuri wasanii wakasomea na taaluma nyingine.
Baada ya katiba mpya kuidhinishwa, ni wazi kwamba wasomi ndiyo watakaokuwa na nafasi ya kupata kazi au tenda, iwe serikalini au kwingineko. Hivyo ni muhimu kujihami, anasisitiza mwimbaji huyo mwenye mtoto mmoja ndani ya ndoa yake. Mtoto huyo anaitwa, Tumisio.

0 comments:

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More

 
Design by Free WordPress Themes | Bloggerized by Lasantha - Premium Blogger Themes | Grants For Single Moms